Wapendwa, kwa heshima na upendo mkubwa tunawakaribisha katika Mkutano Mkuu huu wa tisa wa Konferensi ya Mara. Ni neema kuu ya Mungu iliyotuwezesha kukutana tena pamoja baada ya kipindi cha miaka mitatu. Mungu atukuzwe.
Tunamshukuru Mungu wetu kwa makuu ambayo ametutendea katika kipindi hiki kwa kutuongoza, kutulinda na kuendeleza kazi yake katikati yetu. Kama vile maneno ya nabii Samweli yanavyoshuhudia: “. . . Hata sasa Bwana ametusaidia” (1 Samweli 7:12).
Tunakutana si kwa nguvu zetu, bali kwa rehema zake kuu, tukijua kuwa huu ndio mkutano wa Bwana, na tunapaswa kufanya kila jambo kwa heshima, mshikamano na kwa utukufu wake (1 Wakorintho 10:31).
Mkutano huu uwe mahali pa kusikiliza sauti ya Mungu, kuimarisha mshikamano wa utumishi na kuendeleza kazi yake. Hebu tumruhusu Bwana mwenyewe awe miongoni mwetu, atupe umoja wa Roho, busara na utashi wa kufanya maamuzi kwa ajili ya ustawi wa kanisa lake.
Tusisahau kuwa lengo letu kuu ni moja: kuimarisha kazi ya injili na kuandaa watu kwa ajili ya kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbuka Yesu anakuja, Twendeni!
Karibuni sana, na baraka za Bwana ziwe juu ya kila mmoja wetu.
Mch Joseph J. Matongo
Mwenyekiti wa Mara Conference
Kazi ya Mungu kama ilivyo kazi nyinge katika kampuni/ taasisi nyingine yoyote ili kufanikiwa na kusongeshwa mbele ina hitaji sana rasilimali (Resources). Kanisa hapa konferensi ya Mara Mungu amelipatia rasilimali nyingi ambazo hasa ni kwaajiri ya utume wa wokovu wa mataifa.
Ofisi yetu ya Katibu Muhazini inahusika sana katika kuangalia na kutunza hizi rasilimali ambazo Bwana amelipatia kanisa lake hapa Mara. Tukiziangalia japo kwa uchache rasilimali hizi ambazo ziko katika makundi kadhaa utagundua Bwana amesha tuwezesha.
Kundi la kwanza Rasilimali Watu (Human Resources) Washiriki wa kanisa wenye vipawa, maarifa, na ujuzi. Mtaji wa kazi ya Mungu ni mimi na wewe (Waumini ndani ya kanisa) hivyo tunapaswa kuleana, kutiana moyo, kutembeleana huku tukila chakuala cha roho zetu, na kutumia taranta zetu na vipawa (ambavyo ni tofauti tofauti) kwa kazi ya utume (Warumi 212:6-7, na COL 328)
Kundi wa pili ni Rasilimali Fedha (Financial Resources) Zaka, sadaka na zawadi mbalimbali ni mafuta katika injini ya kuhudumia kanisa, shule, hospitali, kueneza injili ya wokovo na kuwasaidia wahitaji.
Tunaagizwa kusimamia fedha vizuri tangu nyumbani mwetu kwa kumfanya Mungu kuwa wa kwanza, hivyo kupatiwa hekima ya namna ya kutumia fedha ambazo Mungu ameweka mikononi mwetu kama mawakili wake. Tunakumbushwa na kukumbushana kuwa fedha hizi sio mali zetu na siki moja hazitakuwa na thamani mikononi mwetu isipokuwa zile tulizo wekeza mbinguni wa kuwa saidia wenye shida na kuendeleza utume wa wokovu wa mataifa (9T uk 245)
Kundi la tatu ni Rasilimali Mali/ Vifaa (Physical/Tangible Resources) mfano majengo ya kanisa, shule, hospitali, vifaa mbalimbali, vitabu , na technolojia. Hivi vikitumika vyema na kuelekezwa katika utume wa kazi ya Mungu, huchochea ustawi bora sana wa kazi ya Mungu.
Changamoto ni pale mali hizi zinapo telekezwa, majengo ya makanisa huwa kama magofu, nyumba kama mapango, shule kama nyumba za makumbusho, hopitali kama nyumba za waganga wa jadi. Hii huudhalilisha ufalme wa Mungu mkuu n ahata kufungia nje wale ambao wangevutwa kwa kuona ukuu wa Mungu wetu, mali hizi kwa kuwa zilitolewa kwa Mungu ni takatifu kwake. (CE uk 76)
Kundi la nne ni Rasilimali Wakati (Time Resources) Sisi sote tumepewa muda sawa, namna tunavyo tumia muda tulio pewa inaleta tofauti toka mtu mmoja Kwenda mtu mwingine. Mwandiventista wa Sabato katika amri ya nne anaagizwa mambo mawili, moja kufanya kazi kwa siku sita na la pili kupumzika siku ya saba. Wengiwetu wamejikuta wakipenda na kulizungumzia Zaidi jambo la pili, “kupumzika” sasa unawezaje kupumzika bila kuchoka, na unachokaje bila kufanya kazi na Kutenda mambo yote.
Kupoteza Muda bure ni hasara ambayo imesababisha watu wetu kuwa maskini na fukara na kuchangia katika kukosa rasilimali fedha mwishowe hata kazi ya utume inaendeshwa kwa kuchechemea. Ellen white katika COL ana sema tutatoa hesabu ya namna tulivyo tumia Muda (Col: 342)
Kundi la tano ni Rasilimali Maarifa na Habari (Knowledge & Information Resources) Mafundisho sahihi ya Biblia, maandiko ya Ellen G. White, elimu ya vitabu, pamoja na maarifa ya kisayansi na kiutawala, ni utajiri ambao Mungu amelipatia kanisa lake hapa duniani. Ukitumika vyema unasaidia katika utume wa kazi ya wokovu ambayo ni agizo la Mungu kwetu sote (Agizo la Enendeni mkawafanye mataifa…)
Tunapokutana kwenye mkutano huu makini wa kupokea taaria, kutathimini kazi, na kupanga kazi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, tukubali kuwa rasilimali mikononi mwa Mungu. Mungu atatutumia vyema na kwa faida na mafanikio ya kazi ya utume ambao ameuweka mikononi mwetu katika nyakati hizi za mwisho.
Pardon N. Kikiwa
Katibu Mhazini